Kujifunza kupitia ziara za kubadilishana uzoefu kati ya wanajamii kumekuwa muhimu sana katika kuongeza uelewa na maarifa kuhusu suluhisho la changamoto mbalimbali. Kubadilishana huku kunafanyika kati ya wanajamii katika ngazi tofauti—kikundi kwa kikundi ndani ya makazi, katika ngazi ya jiji ambapo jamii kutoka jiji moja husafiri kwenda jiji jingine, na pia katika baadhi ya matukio hutolewa fursa za ziara za kubadilishana uzoefu kimataifa kulingana na mahitaji.

Mbinu hii ya kujifunza imehusisha jamii pamoja na maafisa wa serikali ili kujifunza kutokana na mbinu bora zilizopo ndani na nje ya nchi. Ziara hizi zimekuwa na mchango mkubwa katika kujenga kujiamini kwa jamii, kuwezesha uhamishaji wa maarifa kutoka jamii moja kwenda nyingine, na pia kuwahamasisha maafisa wa serikali kujibu mahitaji ya wananchi.

CCI na Shirikisho la Watu Maskini wa Mijini Tanzania ni sehemu ya mtandao mkubwa wa kimataifa wa jamii za watu masikini mijini unaojulikana kama Slum Dwellers International (SDI). Mtandao huu una wanachama kutoka zaidi ya nchi 38 barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini. Ushirikiano huu umekuwa muhimu sana katika kuongeza upeo wa maarifa kwa wanajamii na maafisa wa serikali kwa kuwapa fursa ya kujifunza kutoka kwa wenzao kuhusu mbinu bora za kukabiliana na changamoto zinazowakabili watu wa kipato cha chini wanaoishi katika maeneo yasiyo rasmi mijini.