Shirika la Centre for Community Initiatives (CCI) linavunia
kushiriki katika Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani
(WMO) kuhusu Utabiri wa hali ya hewa na mabadiliko Tabianchi, uliofanyika
Arusha, Tanzania. Mkutano huu uliwakutanisha wataalamu wa tabianchi,
wanasayansi, watafiti, watendaji wa maendeleo, na wadau mbalimbali kutoka
maeneo tofauti kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha matumizi ya
taarifa za tabianchi katika kufanya maamuzi na kujenga ustahimilivu wa jamii.
Mkutano huu ulitoa fursa muhimu ya kubadilishana maarifa,
kuimarisha ushirikiano kati ya wadau, na kujadili mbinu bunifu za kuboresha
utabiri wa tabianchi na utoaji wa huduma za taarifa za tabianchi zinazokidhi
mahitaji halisi ya jamii.
Katika mkutano huo, CCI iliwasilisha kazi zake zinazoendelea
katika kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na
kuendeleza mikakati ya kukabiliana na athari za tabianchi inayoongozwa na jamii
nchini Tanzania.
CCI iliwasilisha matokeo ya tafiti kuhusu Upimaji wa joto na
uhusiano kati ya matumizi ya nishati kwa ajili ya kupikia na athari za joto
kali ikieleza changamoto zinazokabili jamii zinazoishi katika makazi yasiyo
rasmi. Matokeo hayo yalionesha umuhimu wa kutumia ushahidi unaotokana na jamii
ili kuelewa vizuri athari za joto kali na kusaidia kubuni mikakati jumuishi na
inayozingatia mazingira halisi ya jamii katika kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi.
Aidha, CCI ilishirikisha maendeleo ya Mradi wa DARAJA,
unaolenga kuboresha upatikanaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa na mabadiliko
ya tabianchi kwa jamii. Kupitia mradi huu, CCI inaendelea kuimarisha matumizi
ya huduma za hali ya hewa, mifumo ya tahadhari za mapema, na kuwawezesha
makundi yaliyo katika hatari zaidi ikiwemo wanajamii waishio katika makazi
yasiyopimwa, wakulima, wavuvi, wafugaji na wajasiriamali wadogo kufanya maamuzi
sahihi na kujiandaa vizuri dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa ma tabianchi.
Ushiriki wa CCI katika mkutano huu unaendelea kuimarisha
dhamira yake ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha taarifa za
tabianchi zinapatikana kwa urahisi, kujenga ustahimilivu wa jamii, na kukuza
suluhisho endelevu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Add New Comment