Wafanyakazi wa CCI pamoja na timu ya LOACT (Emanuel Osuteye kutoka Chuo Kikuu cha London – University College London, Vanessa Broto kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield, na Mutafu Manda kutoka Chuo Kikuu cha Mzuzu nchini Malawi) walitembelea jumuiya ya Shaurimoyo Ward Development Society (SHAWADESO) katika Shehia ya Shaurimoyo, Zanzibar.

Ziara hiyo ilifanyika wakati wa mkutano wa utafiti wa LOACT (Action at the Frontline). SHAWADESO ni kikundi cha jamii ambacho kimejihusisha na ukusanyaji wa taka katika kata ya Shaurimoyo tangu mwaka 2000, ambapo Diwani wa Shaurimoyo, Bw. Hassan, ndiye mwanzilishi wa kikundi hicho. Lengo la kikundi ni kuboresha afya ya jamii kupitia uhamasishaji kuhusu usimamizi wa taka, wakiwa wameanzisha harakati ya ukusanyaji taka ambayo sasa imebadilika na kuwa fursa ya ajira kwa wanakikundi, ambapo kila mshiriki hupata kati ya Tsh 50,000 hadi 100,000 kwa mwezi. Kikundi kina jumla ya washiriki 60.

Pamoja na shughuli ya ukusanyaji taka ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa kata ya Shaurimoyo na SHAWADESO, kikundi pia kinatumia taka kutengeneza mboji/mbolea, ambayo nayo imekuwa chanzo kingine cha kipato kwa wanakikundi.